IJUMAA ya leo Novemba 15 timu yetu ya Taifa ya Tanzania itakuwa na kazi ya kumenyana na Equatorial Guinea kwenye mechi ya kutafuta kufuzu michuano ya Chan inayotarajiwa kufanyika 2021.
Ugumu wa michuano hiyo unatakiwa uchukuliwe kwa umakini na wachezaji pamoja na benchi la ufundi kwa kufanyia kazi makosa ambayo yamekuwa yakijirudia kwenye timu yetu ya Taifa.
Ipo wazi kwamba wimbo mkubwa wa siku zote kwa timu ya taifa ni kutokuwa na safu kali ya ushambuliaji jambo ambalo limekuwa likfanya kazi kubwa kwa wachezaji kupata ushindi.
Ikumbukwe kwamba mechi ya nyumbani ni muhimu kwa wachezaji kupata matokeo chanya ambayo yatawafanya wazidi kujiamini kwenye mechi za kimataifa zinazofuata.
Pia ni muhimu kwa ajili ya wachezaji kujiweka sokoni hasa ukizingatia kwamba kwa sasa teknolojia imekuwa kubwa na kila mmoja anafuatilia mechi hasa za kimataifa.
Ni matumaini yangu kwamba mashabiki watajitokeza kwa wingi uwanja wa taifa na wachezaji watafanya kile ambacho wamefundishwa kukifanya kwa umakini.
Kinachohitajika ni nidhamu pamoja na jitihada kubwa kwa wachezaji kutafuta matokeo uwanjani ni kitu ambacho kinatakiwa kuchukuliwa kwa ukaribu na umakini.
Uwepo wa mechi ya kimataifa siku ya Ijumaa pia kumefanya Ligi Kuu Bara kusimama kwa muda kupisha mechi za kirafiki na za kiushindani.
Hii ni kwa mujibu wa kalenda ya Fifa jambo ambalo linaifanya ligi isimame na masuala mengine yaendelee kufanyika kwa wakati ambao umepangwa.
Sasa hapo kuna timu ambazo hazijawa na mwendelezo mzuri kwenye ligi ni wakati wao sasa kutathimini na kutafakari wapi ambapo wanakosea.
Mfano kuna timu ya Singida United mpaka sasa haijaonja ladha ya ushindi ndani ya mechi 11 ambazo wamezicheza kwa sasa za ligi hii ni hatari kwao pamoja na Mbeya City na Ndanda ambao nao wameanza kwa kusuasua kwani wameshinda mechi moja kwa sasa.
Huu ni mfano tu wa timu ambazo zinashiriki ligi kwa sasa huku kinara akiwa ni Simba aliyecheza mechi zake 9 na ana pointi 22
Kuna umuhimu wa kutumia muda huu wa mapumziko kufanyia kazi mapungufu ambayo yemekuwa yakiwasumbua wachezaji pamoja na timu kiujumla.
Viongozi wa timu pamoja na benchi la ufundi ni wakati wa kutulia na kufanya kazi kwa ukaribu kwa kuzingatia yale ambayo yamekuwa yakiwasumbua muda mrefu..
Kama kuna matatizo ambayo yanawamaliza kimyakimya ni wakati wa kuyafanyia kazi ili kuweza kurudi kwenye kasi ya ushindani ambayo inahitajika.
Singida United haijawa na msimu mzuri kwa kipindi hiki sawa na msimu uliopita wa 2018/19 na iliponea chupuchupu kushuka daraja ila safari hii wameanza kupoteana mapema.
Endapo watashindwa kurudi kwenye ubora na kumaliza tofauti zao basi nirahisi kurejea walikotoka mwanzo kwani muda sio rafiki nao kwa sasa wanapaswa wazinduke.
Timu zote kiujumla hata zile ambazo zinaona zinafanya vizuri hakuna haja ya kubweteka kwani ligi bado mbichi na kwa sasa ni mzunguko wa kwanza.
Haina maana kwa kuwa ni mzunguko wa kwanza basi kuna umuhimu wa kwenda kwa mwendo wa kusuasua hapana ushindani ni lazima uwepo muda wote.
Wachezaji mna kazi ya kutafuta matokeo mkiwa uwanjani kwani furaha ya mashabiki ni kuona timu inapata matokeo chanya muda wote.
Licha ya kwamba kwa sasa kumekuwa na mdhamini mkuu bado kumekuwa na taarifa kwamba hawapewi fedha zao kwa wakati basi katika hili kuna umuhimu wa kulitazama upya.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mnapaswa mkae na viongozi wa timu hizi zinazoyumba ili kujua tatizo kwani mna jukumu la kusimamia ubora na mafanikio ya timu zote bila kuzitazama zile ambazo zinafanya vema tu.
Tunaona kwamba kila kitu kinawezekana endapo timu zitaamua kama ilivyo sasa kwa Mtibwa Sugar ambao wameanza kuonyesha dalili za kujiondoa kwenye shimo mapema.
Ikumbukwe kuwa miongoni mwa timu ambazo zilianza kwa kusuasua hata Mtibwa pia ni miongoni mwa hizo hivyo ni suala la maamuzi tu.
Kazi kubwa iwe kwenye kujenga timu na kuifanya iwe na ushindani na sio kushiriki ilimradi unashiriki kila timu ipambane na wachezaji wanatakiwa kujituma kuokoa jahazi la timu.
Post a Comment