Na Saleh Ally, Sousse, Tunisia
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao ametua mjini Sousse hapa Tunisia na kuungana na Kikosi cha Taifa Stars.
Stars ipo mjini hapa kujiandaa na maandalizi ya mwisho kabla ya kuwavaa Libya katika mechi ya kuwania kucheza Afcon, kesho.
Kidao amesafiri kutokea Dubai kuungana na Stars kwa ajili ya mechi hiyo ya pili ya Afcon baada ya ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza dhidi ya Equatorial Guinea jijini Dar es Salaam.
“Nimekuja kuungana na vijana, najua umuhimu wa pointi tatu za ugenini. Limekuwa ni jambo zuri sana kwa kuwa tulishinda mechi ya kwanza.
“Vizuri kama tukifanikiwa kushinda ya pili, tutakuwa tumejiweka katika nafasi nzuri sana. Hivyo nimeona niungane na makocha na wachezaji kwa ajili ya mechi hiyo,” alisema.
Kidao amesema ana imani na maandalizi waliyoyafanya, yaliyobaki yanabaki mikononi mwa makocha na wachezaji na TFF inaendelea kuwaunga mkono bega kwa bega kwa asilimia mia.
Kidao alisafiri na ndege kutoka Dubai hadi Tunis kwa umbali wa saa saba moja kwa moja kabla ya kusafiri kwa saa mbili kwa gari kuja hapa Sousse akiungana na wadau wengine.
Stars imefanya mazoezi kwenye uwanja utakaochezewa mechi dhidi ya Libya kiwania kucheza Kombe la Mataifa Afrika maarufu kama Afcon, kesho.
Kocha Mkuu Ndayiragije, amesema kikosi chake kina hali nzuri na kimejiandaa vilivyo kwa ajili ya mechi hiyo
Post a Comment