JINA la straika wa zamani wa Nkana FC ya Zambia, Walter Bwalya anayekipiga El Gouna FC ya nchini Misri sasa, limetajwa tena kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Bwalya ni kati ya washambuliaji waliokuwa wanatajwa kutua kuichezea Simba kwenye usajili mkubwa wa ligi kabla ya kumsajili mshambuliaji Mbrazili, Wilker Da Silva.
Hesabu za Simba ni kuongeza straika mwingine kwani kwa sasa wanamtegemea Mnyarwanda, Meddie Kagere pekee.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, uongozi huo umepanga kumrudia mshambuliaji huyo kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo ya kumsajili ili kuiimarisha safu yao ya ushambuliaji.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa hilo ni jina la kwanza ambalo limejitokeza kwenye usajili huo wa dirisha dogo, licha ya kuwepo majina mengine lakini Bwalya amekuwa akipewa nafasi kubwa ya kutua Msimbazi.
“Tayari kocha alishaikabidhi ripoti yake ya usajili kwa uongozi katika kuelekea usajili wa dirisha dogo kabla ya usajili wenyewe kuanza, kati ya mapendekezo yake ya kwanza ni kumsajili mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa zaidi ya Kagere na Bocco.
“Hivyo, uongozi umeona urejee kwa Bwalya waliyemkosa kwenye usajili uliopita na kama mambo yakienda vizuri, basi watamalizana naye na kuja kujiunga na Simba,” alisema mtoa taarifa. Aussems hivi karibuni aliliambia Championi Jumatano kuwa: “Lazima tusajili mshambuliaji mwingine mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao kama Kagere aje kutusaidia katika safu yetu ya ushambuliaji kwani waliopo wengine ni majeruhi.
Post a Comment