UONGOZI wa Yanga baada ya kuona uwezekano mdogo wa kumpata mshambuliaji Moses Phiri, sasa umehamia kwa mshambuliaji Ricky Banda mwenye uraia wa Zambia anayekipiga Red Arrows.

Hapo awali Yanga ilikuwa ikihusishwa kwa karibu katika usajili wa mshambuliaji wa Zesco, Moses Phiri ambaye kwa sasa ni wazi ana asilimia kubwa ya kujiunga na Simba.

Katika suala zima la usajili ndani ya Yanga, linasimamiwa kwa asilimia kubwa na wadhamini wao Kampuni ya GSM, chini ya Mkurugenzi Uwekezaji wa GSM ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mashindano Yanga, Injinia Hersi Said.

Habari zimeeleza kuwa timu hiyo ipo katika mazungumzo na mshambuliaji huyo ambaye amekuwa na kiwango bora ndani ya ligi ya Zambia akiwa ndiye kinara wa mabao katika ligi hiyo huku kukiwa na asilimia kubwa ya kumpata mchezaji huyo ambaye mkataba wake unakwenda ukingoni.

“Yanga ina mawasiliano ya wachezaji zaidi ya wawili kutoka Zambia, Moses Phiri lilikuwa ni chaguo la kwanza ndani ya timu lakini kumeonekana kuwa kuna ugumu kumpata mchezaji huyo jambo ambalo limepelekea kuhamisha nguvu zote kumpata Ricky Banda ambaye pia ni mshambuliaji.

“Mchezaji huyo kwa sasa anamalizia mkataba wake ambapo mwishoni mwa mwezi huu utamalizika, mwenyewe ameonyesha nia ya kuondoka na matakwa yake ni kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao jambo ambao lipo kwa Yanga msimu ujao,” kilisema chanzo.

Wakala wa mchezaji huyo kutoka katika Kampuni ya Sepuya Agency, alithibitisha juu ya mteja wake huyo kuwa katika mazungumzo na Yanga.

“Banda ni kweli mkataba wake utamalizika mwishoni mwa mwezi wa sita na tuna ofa nyingi tayari mezani huku mchezaji mwenyewe akithibitisha kuhitaji kucheza katika timu ambayo itakuwa inashiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

“Kuhusu kwa upande wa Tanzania ni Yanga pekee ndio wanamuhitaji mchezaji huyu na kwa sasa tunasubiri kalenda ya FIFA ili michezo ya timu ya Taifa za Zambia imalizike kisha tuendelee na mazungumzo kwa upande wa Yanga,” alisema wakala huyo.

Chanzo:Championi