Kikosi chetu kimeanza safari asubuhi hii kuelekea mjini Songea tayari kwa mchezo wa Jumatano wa kukamilisha msimu wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Mbeya Kwanza.
Kikosi kimeondoka jijini Mbeya baada ya mchezo wa jana kwa basi kikiwa na wachezaji wote tuliosafiri nao kwa ajili ya mechi mbili za Nyanda za Juu Kusini.
Baada ya timu kuwasili Songea wachezaji watafanya mazoezi ya utimamu wa mwili (recovery) baada ya mechi ya jana dhidi ya Tanzania Prisons na kesho tutafanya ya mwisho.
Mchezo wetu dhidi ya Mbeya Kwanza utapigwa Jumatano saa 10 jioni katika Uwanja wa Majimaji.
Mashabiki waliojitokeza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa wamemwagia pesa mlinzi wa kimataifa, Pascal Wawa wakati wa kuagwa baada ya kumalizika mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mchezo wa leo ni wa mwisho kwa Wawa kucheza ndani ya kikosi chetu baada ya kudumu kwa miaka mitano na ulipangwa rasmi kumuaga nyota huyo wa kimataifa kutoka Ivory Coast.
Mashabiki wetu wameonyesha upendo mkubwa kwa Wawa kama ilivyokuwa kwa kiungo mshambuliaji Rally Bwalya ambaye naye alitunzwa pesa.
Tumeweka utaratibu mzuri kwa kuhakikisha tunamalizana vizuri na wachezaji wetu kwa kuwaaga mbele ya mashabiki wetu kutokana na kuthamini michango yao ndani ya klabu yetu.
Mchezo wetu wa mwisho katika Uwanja wa nyumbani wa Benjamin msimu wa 2021/22 dhidi ya Mtibwa Sugar umemalizika kwa ushindi wa mabao 2-0.
Pape Sakho alitupatia bao la kwanza dakika ya 16 baada ya kumalizia pasi ya kisigino iliyopigwa na Kibu Denis.
Peter Banda alitupatia bao la pili dakika ya 44 baada ya kupiga shuti lililokwenda moja kwa moja na kumshinda mlinda mlango wa Mtibwa, Shaban Kado.
Kiungo wa Mtibwa Said Ndemla alitolewa kwa kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 66 baada ya kumchezea vibaya Sadio Kanoute.
Kocha Seleman Matola alifanya mabadiliko ya kuwatoa Denis Kibu na Pape Sakho na Kuwaingiza Yusuf Mhilu na Taddeo Lwanga.
Mtoto wa miaka mitano Bernadetha Joseph Mwamboneke amewawakilisha mashabiki wetu nchi nzima katika hafla ya kuwashukuru kwa kuwa pamoja nasi msimu mzima wa 2021/22.
Uongozi wa klabu umetumia mchezo wetu wa mwisho wa nyumbani tuliocheza na Mtibwa Sugar kuwashukuru mashabiki kwa mchango wao mkubwa waliotupa tangu mwanzo mpaka leo.
Mtendaji Mkuu wa Klabu, Barbara Gonzalez amemkabidhi mtoto Bernadetha jezi maalumu ikiwa na maana ya kuwashukuru mashabiki wote nchi nzima.
Kabla ya kumkabidhi Bernadetha jezi hiyo, Barbara alitembelea vikundi vyote vya hamasa vilivyojitokeza uwanjani kwenda kuwashukuru.
Baada ya kumalizika kwa mchezo Viongozi na Maafisa wa klabu walishuka chini ya uwanja na kuwapungia mashabiki kuonyesha tunawathamini.
Bwalya amesema “Kujiunga na Amazulu kwangu ni mafanikio makubwa kwani nimekuwa nikiitazama na kuifuatilia kwa muda mrefu”
Timu ya Amazulu imemaliza Msimu wa 2021/22 ikiwa nafasi ya 7 katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini kati ya timu 16
Baada ya kutajwa sana kutakiwa na kujiunga baadhi ya klabu za hapa nchini,kiungo Morlaye Sylla wa klabu ya Horoya amejiunga na klabu ya Arouca ya nchini Ureno.
Uongozi wa klabu umempa mkono wa kwa heri mlinzi wa kati Pascal Serge Wawa, raia wa Ivory Coast ambaye anamaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu.
Wawa atacheza mchezo wake wa mwisho akiwa na kikosi chetu Juni 23, dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo tutautumia kumuaga rasmi.
Baada ya mchezo huo, Wawa hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachosafiri kwenda Nyanda za juu Kusini kwa ajili ya mechi zetu mbili zilizobaki za kumalizia msimu dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya Kwanza.
Wawa amedumu nasi kwa kipindi cha misimu minne akituwezesha kuchukua ubingwa wa Tanzania bara mara nne mfululizo, ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports mara mbili, Ngao ya Hisani mara tatu na Kombe la Mapinduzi.
Tukiwa na Wawa tumefanikiwa kucheza robo fainali tatu za michuano ya Afrika ikiwemo robo fainali mbili za Ligi ya Mabingwa na moja ya Kombe la Shirikisho.
Uongozi unapenda kumshukuru Wawa kwa utumishi wake uliotukuka ndani ya klabu yetu na kwa kuthamini mchango wake Alhamisi tutamuaga mbele ya mashabiki kama ilivyo kawaida yetu.
‘Merci beaucoup Pascal Wawa’
Kiungo mshambuliaji Kibu Denis, amesema tuzo ya mchezaji bora wa mashabiki mwezi Mei (Emirate Aluminium ACP Simba Fans Player of the Month) imemuongezea morali ya kuendelea kujituma kuisaidia timu.
Kibu amesema kila mchezaji anafanya jitihada kubwa kufanya vizuri uwanjani kuisaidia timu na kupata tuzo kunaongeza thamani yake.
Pamoja na mambo mengine pia amewashukuru mashabiki waliompigia kura, wachezaji waliompa ushirikiano uwanjani pamoja na benchi la ufundi kwa kumpa nafasi huku akiahidi makubwa zaidi.
“Ni furaha kwangu kama mchezaji kupata tuzo hii. Nawashukuru mashabiki kwa kunipigia kura, wachezaji wenzangu na benchi la ufundi kwa ushirikiano. Hii itakuwa chachu kwangu kuendelea kuipigania timu,” amesema Kibu.
Kwa upande wake Ofisa Mahusiano wa Emirate Aluminium ACP, Issa Maeda amempongeza Kibu kwa kufanya vizuri mwezi Mei na kufanikiwa kuchukua tuzo hiyo baada ya kuibuka mshindi.
Maeda amewaomba wateja waendelee kununua bidhaa za Emirate Aluminium hasa mpya iliyoingia karibuni ya European Style.
“Tumekuja na bidhaa mpya inayojulikana kama European Style au Slide ambayo ni chuma kipya kwa ajili ya kupendezesha nyumba ambacho ni imara chenye muonekano mzuri. Wateja wetu tunaomba muendelee kununua bidhaa zetu ambazo zinaboresha mara kwa mara,” amesema Maeda.
Katika mwezi Mei, Kibu amecheza mechi saba sawa na dakika 630 akifunga mabao matano na kusaidia kupatikana kwa bao moja.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu, Ahmed Ally amesema tutatumia mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya KMC utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku kumuaga kiungo wetu Rally Bwalya ambaye tumemuuza kwa timu moja ambayo itatangazwa baadaye.
Ahmed amesema mchezo wa kesho utakuwa wa mwisho kwa Bwalya ndani ya kikosi chetu kwa kuwa baada ya hapo atarudi nyumbani kwao Zambia kujiandaa kujiunga na timu yake mpya.
Ahmed amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani kuja kuonyesha heshima kwa Bwalya kutokana na mchango wake mkubwa aliutoa kwa timu.
“Jana tulitoa taarifa kuwa tumemuuza kiungo wetu, Rally Bwalya kwa hiyo kesho tutamuaga rasmi katika mchezo dhidi ya KMC kwa sababu baada ya hapo hatacheza tena akiwa na kikosi chetu.
“Niendelee kuwasisitiza Wanasimba wenzangu tujitokeze kwa wingi uwanjani kuonyesha heshima kwa kiungo wetu Bwalya,” amesema Ahmed.
Uongozi wa klabu yetu umefikia makubaliano ya kumuuza kiungo mshambuliaji Rally Bwalya kwa timu ambayo hatutaiweka wazi kwa sasa kutokana na matakwa ya kimkataba.
Bwalya atacheza mchezo wake wa mwisho Jumapili hii dhidi ya KMC na baada ya hapo ataruhusiwa kuondoka kwenda kujiunga na timu yake mpya ambayo inataraji kuanza maandalizi ya msimu (Pre Season) hivi karibuni
Kwa heshima ya mchezaji ambae amedumu nasi kwa misimu miwili tutautumia mchezo wa Jumapili dhidi ya KMC utakaofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa kumuaga rasmi nyota huyo raia wa Zambia
Bwalya alijunga nasi Agosti 2020 kutoka Power Dynamos ya Zambia kwa mkataba wa miaka mitatu ambapo mpaka anaenda kujiunga na timu mpya alikuwa amebakisha kandarasi ya mwaka mmoja.
Kwa misimu miwili aliyodumu nasi Bwalya ameisaidia Simba kushinda mataji matatu ikiwemo ligi kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho la Azam Sports, Kombe la Mapinduzi pamoja na ngao ya jamii
Bwalya pia ameisaidia Simba kufika robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika msimu wa 2020/2021 na Kombe la Shrikisho barani Afrika kwenye msimu wa 2021/2022.
Uongozi wa klabu unamtakia heri Rally Bwalya katika maisha yake mapya ya soka katika timu mpya.
Kaimu Kocha Mkuu, Seleman Matola amewasifu wachezaji kwa kujituma kufanikisha ushindi mnono wa mabao 3-0 tuliopata jana dhidi ya Mbeya City.
Matola amesema tulijua mchezo utakuwa mgumu kutokana na ushindani tunaopata kila tukikutana na City lakini wachezaji walijitahidi kufanikisha ushindi huo.
Matola amesema kipindi cha kwanza tulicheza vizuri tukatengeneza nafasi nyingi lakini wapinzani walikuwa nyuma muda wote ikawa changamoto kuwafungua ingawa tulipata bao moja.
Kiungo huyo wetu wa zamani ameongeza kuwa kipindi cha pili City walivyo funguka kuja kutushambulia tukapata nafasi ya kuwafunga mabao mawili.
“Kwanza tunamshukuru Mungu kwa ushindi huu pili nawapongeza wachezaji kwa kujituma kufanikisha tunapata alama tatu muhimu katika uwanja wa nyumbani.
“Kipindi cha kwanza wapinzani walikuwa nyuma wote kuzuia walipofunguka cha pili tukawafunga mawili,” amesema Matola.
Kikosi chetu kimefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Tulianza mchezo kwa kasi na kuliandama lango la City tukitengeneza nafasi lakini ufanisi wetu katika eneo la mwisho haikuwa nzuri.
Pape Sakho alitupatia bao la kwanza dakika ya 38 kwa mkwaju wa penati baada kufanyiwa madhambi ndani ya 18 na mlinda mlango wa City, Haroun Mandanda.
Kipindi cha pili tulirudi kwa kasi ambapo dakika ya 55 Sakho alitupatia bao la pili baada ya kupokea pasi ndefu ya Mzamiru Yassin na kuwazidi mbio walinzi wa City kabla ya kumpiga chenga Mandanda.
Peter Banda alitupatia bao la tatu dakika ya 76 akimalizia pasi safi ya Yusuf Mhilu kufuatia shambulizi aliloanzisha mwenyewe.
Kocha Seleman Matola aliwatoa Sakho, Kibu Denis, Mzamiru na Bwalya na kuwaingiza Medie Kagere, Banda, Mhilu na Taddeo Lwanga.
Klabu yetu imefanikiwa kumsajili mshambuliaji Moses Phiri raia wa Zambia aliyekuwa anachezea Zanaco FC ya nchini humo kwa mkataba wa miaka miwili.
Phiri ambaye pia anaweza kucheza nafasi za kiungo mshambuliaji na winga zote mbili atavaa jezi nyekundu na nyeupe kuanzia msimu ujao wa mashindano.
Phiri ni usajili wetu wa kwanza kuelekea maboresho makubwa ya kikosi chetu ambayo tumepanga kuyafanya kuelekea msimu mpya unaotarajiwa kuanza mapema hivi karibuni.
Msimu uliopita akiwa na Zanaco Phiri amefunga mabao 14 kwenye ligi kuu ya Zambia akiwa ni mfungaji bora namba mbili nyuma ya kinara mwenye mabao 16
Kaimu Kocha Mkuu Seleman Matola, amesema maandalizi yamekamilika kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Mbeya City utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku.
Matola amesema kikosi kimefanya mazoezi kwa wiki mbili na kimekamilika baada ya wale waliokuwa kwenye majukumu ya timu za taifa kujiunga pamoja na wenzao.
Matola ameweka wazi kuwa sisi ni timu kubwa na tunahitaji kushinda kila mchezo uliopo mbele yetu ikiwemo wa kesho bila kujali tunapambania ubingwa au la.
“Tuko tayari kwa mchezo wa kesho mchezo wa kesho, wachezaji wapo kwenye hali nzuri maandalizi yamekamilika na tuna imani tutapata alama zote tatu.
“Tunaiheshimu Mbeya City, inatupa ushindani mkubwa tukikutana nayo lakini tupo tayari kukabiliana nao kulingana na maandalizi tuliyofanya,” amesema Matola
Klabu yetu leo imekabidhiwa Tuzo ya Klabu Bora ya Kigitali kutokana na kufanya vizuri katika mitandao ya kijamii mwaka 2021.
Tuzo hiyo tumekabidhiwa na waandaaji Serengeti Byte baada ya kuzishinda timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu ya NBC ambazo ni Azam FC, Mbeya City, Ruvu Shooting na Yanga.
Kwa mujibu wa Serengeti Byte, klabu yetu imekuwa na muendelezo mzuri katika Kitengo chetu cha Habari na Mawasiliano na tunafanya vizuri katika mitandao ya kijamii ikiwa na maana ya kwenda na wakati.
Mpaka sasa tunapatikana katika majukwaa mbalimbali katika mitandao ya kijamii ambayo ni Instagram, Facebook, Twitter na Tiktok.