Kikosi chetu kimeanza safari asubuhi hii kuelekea mjini Songea tayari kwa mchezo wa Jumatano wa kukamilisha msimu wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Mbeya Kwanza.
Kikosi kimeondoka jijini Mbeya baada ya mchezo wa jana kwa basi kikiwa na wachezaji wote tuliosafiri nao kwa ajili ya mechi mbili za Nyanda za Juu Kusini.
Baada ya timu kuwasili Songea wachezaji watafanya mazoezi ya utimamu wa mwili (recovery) baada ya mechi ya jana dhidi ya Tanzania Prisons na kesho tutafanya ya mwisho.
Mchezo wetu dhidi ya Mbeya Kwanza utapigwa Jumatano saa 10 jioni katika Uwanja wa Majimaji.
Mashabiki waliojitokeza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa wamemwagia pesa mlinzi wa kimataifa, Pascal Wawa wakati wa kuagwa baada ya kumalizika mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mchezo wa leo ni wa mwisho kwa Wawa kucheza ndani ya kikosi chetu baada ya kudumu kwa miaka mitano na ulipangwa rasmi kumuaga nyota huyo wa kimataifa kutoka Ivory Coast.
Mashabiki wetu wameonyesha upendo mkubwa kwa Wawa kama ilivyokuwa kwa kiungo mshambuliaji Rally Bwalya ambaye naye alitunzwa pesa.
Tumeweka utaratibu mzuri kwa kuhakikisha tunamalizana vizuri na wachezaji wetu kwa kuwaaga mbele ya mashabiki wetu kutokana na kuthamini michango yao ndani ya klabu yetu.
Mchezo wetu wa mwisho katika Uwanja wa nyumbani wa Benjamin msimu wa 2021/22 dhidi ya Mtibwa Sugar umemalizika kwa ushindi wa mabao 2-0.
Pape Sakho alitupatia bao la kwanza dakika ya 16 baada ya kumalizia pasi ya kisigino iliyopigwa na Kibu Denis.
Peter Banda alitupatia bao la pili dakika ya 44 baada ya kupiga shuti lililokwenda moja kwa moja na kumshinda mlinda mlango wa Mtibwa, Shaban Kado.
Kiungo wa Mtibwa Said Ndemla alitolewa kwa kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 66 baada ya kumchezea vibaya Sadio Kanoute.
Kocha Seleman Matola alifanya mabadiliko ya kuwatoa Denis Kibu na Pape Sakho na Kuwaingiza Yusuf Mhilu na Taddeo Lwanga.
Mtoto wa miaka mitano Bernadetha Joseph Mwamboneke amewawakilisha mashabiki wetu nchi nzima katika hafla ya kuwashukuru kwa kuwa pamoja nasi msimu mzima wa 2021/22.
Uongozi wa klabu umetumia mchezo wetu wa mwisho wa nyumbani tuliocheza na Mtibwa Sugar kuwashukuru mashabiki kwa mchango wao mkubwa waliotupa tangu mwanzo mpaka leo.
Mtendaji Mkuu wa Klabu, Barbara Gonzalez amemkabidhi mtoto Bernadetha jezi maalumu ikiwa na maana ya kuwashukuru mashabiki wote nchi nzima.
Kabla ya kumkabidhi Bernadetha jezi hiyo, Barbara alitembelea vikundi vyote vya hamasa vilivyojitokeza uwanjani kwenda kuwashukuru.
Baada ya kumalizika kwa mchezo Viongozi na Maafisa wa klabu walishuka chini ya uwanja na kuwapungia mashabiki kuonyesha tunawathamini.